Kitu pekee kilichokuwa akilini mwa Dk. Ringo ilikuwa ni hatari, alijua wazi kuwa kulikuwa na hatari iliyokuwa mbele yake. Kuwaruhusu maaskari wakague gari lake kulimaanisha kuonekana kwa Dk. Othman jambo ambalo lingesababisha wote kuishia jela! Akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu.
“Mimi ni Daktari wa Muhimbili jamani, mbona hivyo?” Alisema kwa sauti ya chini huku macho yake yakisoma woga aliyokuwa nao.
“Hatuna haya ya kujua kazi yako!” “Bali?” “Tunataka upaki gari lako pembeni kwa ajili ya ukaguzi!” “Huu ni ukaguzi wa aina gani kwa gari langu pekee, kwani hakuna magari mengine ya kukaguliwa zaidi ya hili?” “Usitufundishe kazi, kwanini unazidi kubisha?” “Kwa sababu nimeshawaambia kuwa nachelewa ndege, mgonjwa wangu anatakiwa kusafiri haraka kwa ajili ya kwenda kufanyiwa upasuaji!” “Unapaki gari pembeni au nipasue tairi la gari lako?” Mmoja wa maaskari alisema huku akilenga tairi la mbele la gari la Dk. Ringo kwa bunduki.
Hapo sasa akajua hapakuwa na utani katika jambo hilo, ilikuwa lazima afikirie jambo la kufanya haraka, hakuwa na jibu la kuwapa maaskari wale walioonekana kuwa makini na kazi yao.
Punde taa zikaruhusu magari kupita, lakini kwa kuwa hakuruhusiwa kuondoka akasababisha foleni ndefu ambapo honi zilisikika zikilia kwa sauti kubwa. “Tafadhali naomba mniruhusu!” “Wewe ni mjanja sio?” “Hapana!” “Basi, paki gari pembeni!” Hakuwa na ujanja tena, akakata kulia kisha akaegesha gari pembeni.
Tayari watu walikuwa wameshazunguka eneo la tukio kuangalia kilichokuwa kikiendelea. Askari mmoja akaingia ndani ya gari na kuanza upekuzi kila mahali garini. Dk. Ringo akaamriwa afungue buti, kisha ukaguzi ukaendeelea.
“Shuka chini!” Askari mmoja akamwambia Dk. Ringo “Hakuna tabu!” Dk. Ringo akashuka akionyesha huzuni, uso wake ulionyesha wasiwasi sana.
Hakuwa na kitu kibaya ndani ya gari lake, lakini tatizo lilikuwa ni Dk. Othman ambaye magazeti yote ya siku hiyo, yalikuwa yameandika kuwa alikuwa amejinyonga. Hilo aliliomba kwa sauti ya chini, alijua ni kiasi gani mambo yangeharibika kama Dk. Othman angeonekana akiwa katika gari lake. Akiwa amekaa kimya akisubiria kuambiwa chochote kutoka kwa maaskari waliokuwa wakikagua gari lake, akasikia sauti ya ukali kutoka kwa askari mmoja.
“Mwambie na mwenzako ashuke!” “Huyo ni mgonjwa hataweza!” “Sasa anawezaje kusafiri peke yake mpaka Uingereza?” “Haendi peke yake, nasafiri naye, lakini uwanjani kuna mtu atakayerudisha gari nyumbani!”
Ukaguzi ukaendelea kwa dakika tatu, hawakukuta kitu kibaya! Hatimaye wakamruhusu Dk. Ringo kurudi kwenye gari, akapanda na kuwasha kisha safari ya kuelekea Uwanja wa Ndege ikaendelea. *********
Kila wakati Dk. Ringo alikuwa akiangalia nyuma kupitia vioo vya pembeni vya gari lake kuangalia kama alikuwa akifuatiliwa na gari la polisi, hakuamini kuwa ni kweli alikuwa ameachiwa baada ya ukaguzi na rafiki yake hakugundulika! Huo ulikuwa ukweli ambao hakuwa tayari kuuamini haraka.
“Siamini!” Dk. Ringo alimwambia Dk. Othman. “Hata mimi pia!” “Hakika Mungu ni wa ajabu sana!” “Sana, tena apewe sifa!” “Kazi iliyobaki ni moja Tu!” “Ipi?” “Kufika Uingereza!” “Ni kweli kabisa, kwa uweza wa Mungu hilo linawezekana!” Hawakuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kuendelea na safari ya kwenda Uwanja wa Ndege. Baada ya muda mfupi kidogo wakafika uwanjani, kwa kuwa kila kitu kilikuwa tayari, hawakuwa na muda wa kupoteza.
Muda ulipowadia, Dk. Othman akajiandaa kuingia katika chumba maalum cha ukaguzi kabla ya kuingia kwenye ndege. Akamwangalia Dk. Othman mara mbilimbili, machozi yakaanza kumlengalenga machoni mwake.
“Sijui nikushukuru kiasi gani rafiki yangu?” “Usijali…kuniambia ahsante tu, inatosha!” “Nashukuru kusikia hivyo!” “Safari njema, ila ukifika tu, lazima uwasiliane nami!” “Hakuna shida!” “Emmanuel atakupokea uwanjani, atakuwa mwenyeji wako kama nilivyokuambia, maagizo yote nimeshampatia, kwa hiyo unapaswa kumsikiliza yeye kwa kila kitu!” “Hakuna tabu!” Wakakumbatiana kwa furaha na kuagana. Othman akaingia katika chumba maalum cha ukaguzi, baadaye akaingia ndani ya ndege. Dk. Ringo alisubiri mpaka ndege ilipopaa na kuishilia angani. *********
Dk. Othman aliposhuka tu, uwanjani, akaona bango kubwa lililoandikwa ‘Karibu Uingereza Dk. Mkambila’, Othman alishafahamu kuwa ni yeye ndiye aliyekuwa akisubiriwa! Jina la Mkambila ni jina jipya ambalo walikubaliana kulitumia kuanzia akiwa Tanzania. Mara moja akamfuata mtu aliyekuwa amebeba bango hilo, akamsalimia na kujitambulisha.
“Habari yako ndugu!” “Njema sana!” “Naitwa Othman!” “Naitwa Emmanuel, karibu sana Uingereza!” “Nashukuru sana!” Wakaondoka moja kwa moja mpaka kwenye gari lake, safari ya kuelekea nyumbani kwa Emmanuel ikaanza. Hapakuwa mbali sana na uwanjani, kiasi cha dakika thelathini na tatu tayari walishafika katika nyumba nzuri iliyovutia, nyumba aliyokuwa akiishi Emmanuel.
“Karibu sana ndugu yangu!” “Ahsante sana, nyumba yako nzuri sana!” “Ahsante, hata hivyo sio yangu ni nyumba ya shirika!” “Pamoja na hivyo ni nzuri pia!” “Nashukuru sana!” Wakaingia ndani, akakaribishwa katika sebule nzuri ya kisasa. “Naomba nikuletee kinywaji!” Msichana wa kazi wa Emmanuel alimwambia Othman. “Nashukuru sana, niletee maji ya matunda!” Yule msichana hakuuliza swali lingine, alitoka moja kwa moja mpaka kwenye jokofu kubwa, akatoa maji ya matunda ya mananasi.
“Karibu ufurahie kinywaji!” “Ahsante sana!” Ilikuwa nyumba nzuri sana ya kuvutia, geti imara na mlinzi ilifanya nyumba hiyo kuwa na ulinzi wa kutosha. Emmanuel alikuwa ni Daktari, alisoma na Dk. Ringo miaka ya nyuma, urafiki wao ulikuwa kwa kasi, kiasi wakawa kama ndugu.
Alikuwa akifanya kazi katika Hospitali moja ya Mifupa iliyokuwa jijini London Uingereza. Baada ya kumaliza kupata kinywaji, mazungumzo yakaendelea. Dk. Othman akamweleza kila kitu bila kumficha. Historia yake ilitisha, ingawa alishaelezwa kila kitu na Dk. Ringo lakini kumsikia moja kwa moja akisimulia mkasa unaomuhusu yeye mwenyewe, ulimshtua sana.
“Pole sana ndugu yangu!” “Nashukuru!” “Usijali, kila kitu kitakuwa sawa, hapa kuna wataalamu wazuri sana wa kubadilisha sura za bandia, utakuwa mtu mwingine saa chache zijazo!” “Kweli?” “Kabisa…hakuna atakayekutambua tena, utakuwa mwingine na jina lako litakuwa lingine pia, kitu cha kufurahisha zaidi, uraia wako pia utabadilika, nitakutafutia uraia wa hapa Uingereza!” “Nitafurahi sana!” “Anza kufurahi sasa hivi!” “Nashindwa kuelewa namna ya kukushukuru!” “Usijali ndugu, sisi wote ni wanaume na mambo kama haya yanaweza kumkuta mtu yeyote, ni bora uishi kama mtu mwingine sasa hivi, kuliko kuishia jela au kunyongwa!” “Ni kweli kabisa!” Mazungumzo yakaendelea, kila mmoja akimuuliza maswali mwenzake kwa ajili ya kufahamiana zaidi! Ikiwa ni dakika arobaini na tano tu baada ya Dk. Othman kuingia katika nyumba ya Dk. Emmanuel, akatokea msichana mmoja mrembo sana, alikuwa akitokea katika mlango kubwa wa kuingilia ndani.
Kwa alivyoonekana hapakuwa na ubishi kuwa alikuwa akitokea kazini! Alikuwa mrembo sana, lakini urembo aliokuwa nao, haukumfanya Dk. Othman ashtuke, ila kuna jambo lingine lililotaka kuharibika! Alimfahamu vizuri sana msichana huyo, kitendo cha msichana huyo kugundua kuwa Dk. Othman alikuwa Uingereza, kulimaanisha maisha yake kurudia jela. Akamwangalia kwa macho yaliyojaa huruma na wasiwasi, woga ukiwa umemjaa moyoni mwake! Hakuweza kujua mara moja ni kitu gani kitakachotokea mbele yake, ila aliwaza jambo tu, hatari!
Msichana huyo ni nani na ana nini? Kwanini Dk. Othman ameshtuka baada ya kumuona? Usikose kufuatilia katika gazeti hili siku ya Ijumaa…
|