
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho kiliomba hifahi ya jina lake, baada ya vinara hao kujizolea umaarufu katika tasnia hiyo, hasa baada ya kufanya vizuri katika Filamu ya Johari, wamekuwa hawapikiki chungu kimoja.
Habari zaidi zinasema baada kutoa filamu zao, mmoja kati ya mastaa hao anajiona wa ghali sana kiasi cha kuamua kuanzisha chuki zisizo na sababu.
"Unajua ...(anataja jina) ni mkorofi sana, lakini mwenzake mara kadhaa amekuwa akiomba wakutane kwa ajili ya kuweka mambo sawa, na yeye hukataa," kilieleza chanzo hicho.
Inadaiwa kuwa, baada ya kuwepo kwa maneno ya chini chini kuwa wawili hao sasa ni sawa na paka na panya, waliamua kuyamaliza kisha kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa hawana tofauti yoyote, lakini baada ya muda mfupi 'bifu' likarudi tena upya.
Aidha kiliendelea kupasha kuwa, bifu lililorudi kwa mara ya pili, lilikuwa la kimya kimya huku wawili hao wakikosa hata mawasiliano ya kawaida kama wasanii wa tasnia moja.
"Huwezi kuamini hata kusalimiana kwao ni shida, mimi nakuambia haya kwa uhakika kwa sababu ni watu wangu wa karibu, nawajua vizuri. wanaweza hata kukutana barabarani lakini wapishane kama hawajuani, yaani hawa watu hawapatani hata kidogo," kilieleza chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, chanzo chetu kilipasua kuwa, baada ya bifu hilo kuendelea chini kwa chini, walifikia hatua ya kutumiana meseji za matusi na kutishiana maisha.
"Kuna wakati hutambiana magari, mavazi na vito vya thamani, lakini mambo yamezidi kuwa mabaya baada ya mmoja wao kumtishia mwenzake kumwendea kwa mganga wa kienyeji, ili kumzima nyota yake," kilipasha chanzo hicho.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mmoja wa wasanii hao kutishiwa uchawi, hakuonyesha kujali, badala yake alijibu mapigo kwa kumwambia kuwa angemwendea kwa mtaalam mkali zaidi yake.
"...(anamtaja jina) hakukubali kushindwa, alimwambia kuwa yeye ana mtaalam mzuri zaidi Bagamoyo na kuahidi kupambana naye," kilisema chanzo hicho.
Baada ya gazeti hili kupata madai hayo, lilifanikiwa kumpata Ray kwa njia ya simu ambaye alikasirishwa sana na tuhuma hizo.
"Hivi una akili kweli wewe? Mimi niko ndani ya Yesu, sina mambo ya kishirikina na wala sijawahi kufikiria, kuhusu Kanumba sipo tayari kuzungumza chochote," Ray alisema kwa ukali kisha akakata simu.
Akizungumza na Ijumaa kwa njia ya simu, Kanumba alisema hana muda wa kuzungumzia mambo ya Ray na kwamba ushirikina anausikia kwa watu.
"Mambo ya uchawi na mimi yametokea wapi tena? Mimi nimezaliwa katika familia yenye maadili na inayomwogopa Mungu, sina habari kabisa na mambo ya kishirikina. Kuhusu Ray, sina muda wa kuzungumza juu ya mambo yake," alisema Kanumba kabla ya kukata simu.