
Mara baada ya mkewe Richard kuondoka kwa hasira nyumbani kwa mzee Bezuidenhout usiku wa fainali za BBA, alikwenda kwa rafiki yake mmoja aliyesoma nae Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aishiye maeneo ya Mbezi Beach ambako mumewe hakupajua hadi siku chache zilizopita.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari cha kuaminika, Richard alifanya jitihada za ziada kujua sehemu alikokimbilia mkewe na alipofanikiwa kupajua alikwenda kumuangukia na hatimaye alifanikiwa kumuhamishia kwa siri hoteli aliyofikia.
Katika uchunguzi wake na kwa kusaidiwa na chanzo chake cha habari, Ijumaa limefanikiwa kuibua maficho ya wawili hao ambapo sasa inajulikana wanaishi Holiday Inn, ambayo ni hoteli yenye hadhi ya nyota 5 iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam ambako mshindi huyo wa BBA ndiko alikofikia tangu awasili nchini wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, baada ya mtafaruku uliotokea kati ya Richard na mkewe ambaye alikerwa na uhusiano wa kimapenzi uliokuwepo baina ya ‘Big Brother’ huyo na mshiriki mwenzake kutoka nchini Angola, Tatiana, hivi sasa mambo ni shwari ingawa Ricki hajamtamkia wazi Richard kuwa amemsamehe kwa yote aliyoyafanya.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, ingawa wanafamilia walichukizwa na kitendo cha Ricki kumuita ndugu yao Nguruwe, kauli ambayo ilimaanishi hata yeye ameolewa na nguruwe, lakini kwa sasa wamemsamehe na wamemuomba naye amsamehe mumewe na kwamba yaliyopita yamepita wagange yajayo.
“Kama Ricki aliweza kumuita Richard nguruwe, hiyo ilimaanisha nyumba nzima ni ya nguruwe na bila shaka yeye pia ameolewa na nguruwe. Lakini yote hayo tumemsamehe, hivyo tunamuomba naye amsamehe mumewe, yaliyopita yamepita, tugange yajayo,” kilisema chanzo hicho kikikariri tamko la familia.
Aidha, chanzo chetu kimeeleza kuwa wanafamilia wametoa darasa kwa wanandoa hao kuwa hawana budi kuweka pembeni tofauti zao ili kuinusuru ndoa yao changa ambayo haijaaliwa kupata mtoto hata mmoja.
Katika hatua nyingine, mashabiki wa Richard kutoka sehemu mbalimbali za Afrika, wamekuwa wakimtumia barua pepe kumueleza tabia za Tatiana ambaye alikuwa mpenzi wake kwenye Jumba la BBA.
Mashabiki hao wamemtaka Richard kuanchana kabisa na Tatiana kwani nchini kwao Angola anajulikana kama mwanamke ambaye hajatulia na amepachikwa jina la Kicheche!.
“Kitendo cha Richard kurejea nchini na kutoonana na mkewe, kilimkosesha raha ndiyo maana wakati akiongea na waandishi wa habari alisema atafanya kila awezalo kuhakikisha anampata na kweli amefanikiwa,”ilielezwa.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka kwa mnyetishaji wetu zilisema kuwa baada ya Richard kumpata mkewe, ameamua kuishi naye kwa muda hotelini wakifurahia matunda ya ushindi alioupata.
“Ricki hivi sasa hana kinyongo tena na mumewe kwani amekuwa akienda kuwasalimia wakwe zake kisha kurejea hotelini, sasa roho ya Richard imetulia kwani alitueleza ushindi wake usingekuwa na maana bila kuwa na mkewe,” kilitanabahisha chanzo hicho.
Mshindi huyo wa BBA alikuwa katika mgogoro mkubwa na mkewe, kufuatia kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Tatiana kutoka Angola ambao ulimkera Ricki ambaye inadaiwa aliamua kufungasha virago na kurudi kwao Canada.