arrowSet HomePage |arrowBookMark Us
right
lines

Global Publishers Tanzania- Uwazi » hadithi za Shigongo » MY GHOSTS (MIZIMU YANGU – 37 )

Tafuta  

Tembelea...

Kalenda

Gazeti la Ijumaa

Marafiki wetu

Habari Zilizopita

Soma Magazeti Yetu...

Gazeti la Risasi Mchanganyiko
Amani
Gazeti la Ijumaa Wikienda

Bongo Celebrities ...

 
Habari Zinazotamba Habari Mchanganyiko
» Mpenzi mwenye tabia hizi m ...
» (SIMULIZI ZA CHUMBANI) MDUA ...
» Mduara wa Mahaba (19)
» (SIMULIZI ZA CHUMBANI) MDUA ...
» Aisha Madinda: NGONO INANIU ...
» JACKLINE AMUANIKA ALIYEMTOA ...
» KANUMBA: NARGIS ALINITESA ...
» Latoya amechafuka Tanza ...
» Yanga SC ni noma
» Kitu mbaya
» Nyoshi sasa kuporwa vit ...
» Kwanini mnashika Msahaf ...
» Michael Richard Wambura
» MAMBO HAYA HUMBOA MWAND ...

MY GHOSTS (MIZIMU YANGU – 37 )

hadithi za Shigongo

Kanisa zima lilishangilia ukuu wa Mungu ulivyokuwa wa ajabu, haikuwa rahisi kuamini msichana mzuri kama Jeniffer alikuwa jini kabla, tena asubuhi tu ya siku hiyo walikuwa wametoka chini ya bahari. Vilegelegele vikaendelea kuridhima na kila mmoja kwa wakati wake alikuwa akitamka neno la kumsifu Mungu.

Jeniffer alikuwa amesimama, akiendelea kusimulia historia ya maisha yake huku akilia, akinamama walimsogelea na kumfuta machozi.

“Nimefanya dhambi nyingi sana katika maisha yangu, niliua watu wengi sana wasio na hatia, kuanzia nilipokuwa mdogo nasoma. Nimeshasababisha ajali nyingi sana, yote ni kwa ajili ya kuwapelekea majini damu! Hakika sikutamani hata kidogo maisha hayo, lakini nililazimishwa na sikuwa na njia ya kupambana nayo.

“Wakati mwingine nilipokuwa na kiu ya kumjua Mungu na kutaka kwenda Kanisani, kabla sijafika, nilianguka na kupoteza fahamu njiani, lakini leo hii Yesu Kristo wa Nazareth ameniweka huru!” Jeniffer aliongea kwa hisia huku akilia machozi. Kwa Osward ulikuwa muujiza wa ajabu sana, hakuamini kama Jeniffer angeweza kutamka neno ‘Yesu Kristo wa Nazareth’ siku moja.

“Yesu ndiye aliyenikoa!” Jeniffer alisema kwa mara nyingine.
“Aaaamen....” Kanisa liliitikia.

“Kuanzia leo nimefunguliwa vifungo vya shetani na nimeanza kuishi maisha mapya bila bugudha za ibilisi!”
“Haleluyaaaa!” Mchungaji Deo Lubala alisema kwa sauti.

“Ameeen....” waumini wakaitikia. Ilikuwa jioni ya ajabu kanisani pale, wakati yote hayo yakitokea, Osward alibaki kimya akibubujikwa na machozi mashavuni mwake.

Alijiona mshindi wa mambo mawili, kwanza kuweza kumtoa Jeniffer katika utumwa wa shetani na pili, kumpata mwanamke aliyempenda kwa moyo wake. Kwake ilikuwa furaha ya ajabu ambayo haikuwahi kutokea katika maisha yake.

“Namshukuru sana mchumba wangu Osward, bila yeye nisingekuwa huru leo!” Jeniffer alisema kisha yeye na Osward wakatoka mbele baada ya Mchungaji Lubala kutoa ishara waende mbele. Walipofika akawataka wapige magoti chini, kisha mchungaji akawageukia waumini, kisha akaanza kuzungumza taratibu kwa hisia kali za kiroho, alionekana kuzama ndani kabisa ya ulimwengu wa watakatifu.

“Haya njooni tusemezane, asema Bwana wa Majeshi; dhambi zenu zijapokuwa nyekundu kama bendera zitakuwa nyeupe kama sufi, zijapokuwa nyekundu kama damu zitakuwa nyeupe kama theluji. Mungu wetu ni mwema sana, ameweza kumtoa dada yetu Jeniffer katika kifungo cha shetani na kumweka huru leo, hakika sasa amekuwa kiumbe kipya!

Naomba wazee wa kanisa waje hapa, tuungane pamoja tuwawekee mikononi Jeniffer na Osward, wengine mnaweza kuwaombea huko huko mlipo!” Mchungaji Lubala alisema huku akishuka madhabahuni na kuwasogelea Jeniffer na Osward waliokuwa wamepiga magoti chini ya madhabahu. Wazee wa Kanisa hawakuchelewa kufika na kuwawekea mikono, maombi yakafanyika na baadaye wakarudi kuketi.

Taratibu nyingine zikaendelea hadi ibada ilipoisha saa 1.00 usiku! Wakati wa kuagana, Mchungaji Lubala akawaita Jeniffer na Osward pembeni.

“Osward Mungu akubariki sana, una kila sababu ya kumshukuru Mungu, nimeupenda ujasiri wako, endele kumwomba Mungu zote za maisha yako, kuna kitu ndani yako siku moja Mungu mwenyewe atakidhihirisha!”
“Nashukuru kusikia hivyo Mchungaji!”
“Kitu kingine ni kwamba, Jeniffer anatakiwa kuanza mafundisho ya Biblia mara moja, ili abatizwe na baadaye mfunge ndoa!”

“Nipo tayari kuanza hata kesho Mchungaji, nina hamu sana ya kumjua Mungu!” Jeniffer alisema.
“Nafurahi kusikia hivyo, mwalimu wako wa kwanza ni Osward, na ningependa wiki ijayo uanze mafundisho ila usikose ibada zetu zote, kuanzia Fellowship hadi ibada za kawaida za jumapili!”
“Siwezi kukosa hata siku moja Mchungaji!” Jennifer alijibu.

‘Nitahakikisha anahudhuria kila ibada Mchungaji!” Osward akadakia.
“Nafurahi sana kusikia hivyo, ila kuna kitu kimoja muhimu mnatakiwa kuzingatia!”
“Kitu gani Mchungaji?” Osward akauliza akionyesha wasiwasi kidogo.

“Shetani ni mdanganyifu sana, kazi yake ni kuwalinda walio katika himaya yake wasitoke, lakini pia kuwadanganya walioijua kweli. Hivyo basi yawapasa muwe waangalifu, msivunje amri ya Mungu hadi siku mtapoungana na kuwa mwili mmoja!” Mchungaji alisema, hakuna ambaye hakuelewa alichomaanisha, wakaangaliana kisha wakakumbatiana na kuachiana baada ya sekunde kadhaa.

“Mchungaji siku zote nasimama katika imani yangu, siwezi kufanya hivyo. Isitoshe Jeniffer ni wangu tu, kwanini niwe na haraka naye?”
“Haleluyaaa....”
“Amen!”
*********
Ilikuwa saa 2.00 usiku, Osward na Jeniffer wakiwa sebuleni wakiangalia taarifa ya habari ya kwenye Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten. Walikuwa nyumbani kwa Jeniffer Oysterbay, pembeni kukiwa na glass za maji ya matunda. Walikuwa wakinywa kwa furaha huku Jeniffer akizidi kumshuru Osward kwa kumtoa katika utumwa wa dhambi.

“Kama siyo wewe, ningeendelea kuteseka daima, ahsante sana Osward!”
“Siyo mimi ninayestahili sifa hizo Jeniffer!”
“Ni nani sasa?”

“Mungu pekee, maana yeye ndiye Yohava!”
“Amen!” Maisha yakabadilika, Jeniffer akazoea jina la Yesu na kila kitu kinachomhusu Mungu alikuwa akiitikia Amen! Hakusikia kizunguzungu wala dalili za kudondoka tena, kwake jina la Yesu lilikuwa na nguvu za ajabu.
“Sasa mpenzi kuna kitu nataka kukuambia!”
“Kitu gani?”

“Ni kuhusu siku ya harusi yetu!”
“Mh! Mapema sana kuizunguzia!”
“Mapema?” Jeniffer akabadilika kidogo, Osward alikuwa ameshamuingia akilini, hakuhitaji kitu kingine zaidi ya ndoa.

Tamaa za mwili wake ziliwaka, alitamani sana kuwa kitandani na Osward, kama walivyozaliwa wakicheza mchezo wa watu wazima. Kitendo cha Osward kujibu kuwa ni mapema sana kuzungumzia ndoa yao kilimuudhi sana. Osward aligundua hilo.

“Nimekuudhi?”
“Kwahiyo unadhani umenifurahisha sio?”
“Basi mpenzi, nilikuwa nafanya utani tu! Naomba unisamehe malkia wa moyo wangu!” Hilo lilikuwa neno pekee ambalo lingeweza kumrudishia Jeniffer tabasamu lililopotea! Alikuwa amekasirika na uso kukunjamana, jambo ambalo Osward hakulipenda.

“Utani mwingine sio mzuri Osward!”
“Usijali, sasa?”
“Nini tena mpenzi wangu?”
“Nataka kwenda!”
“Wapi?”

“Nyumbani kwangu!”
“Osward....”
“Unasemaje mpenzi!”
“Unataka kuniudhi sasa?”
“Kwanini tena, si nilikuwambia nilikuwa nakutania?”
“Najua lakini sizungumzii hayo tena!”
“Kumbe lipi jipya?”

“Siwezi kulala peke yangu Osward, lazima nilale na wewe mpenzi wangu!” Jeniffer alikuwa katika mapenzi mazito sana kwa Osward, kulala peke yake kwa muda huo, ilikuwa ni sawa na kukosa chakula! Alimpenda sana Osward.
“Hilo tu?”
“Kwani dogo?”
“Basi mpenzi, tutalala pamoja!” Muda huo huo Jeniffer akamkumbatia Osward na kumbusu mfululizo, kabla ya kumtaka asimame.

“Karibu mezani mume wangu, chakula kipo tayari!”
“Ahsante!” Wakaongoza hadi mezani, wakaketi na kuanza kula kwa furaha. Wakati mwingine walikuwa wakilishana, Jeniffer alifika mbali zaidi, alikuwa akiweka chakula kinywani mwake, kisha baada ya kutafuna humlisha Osward kwa mdomo!

“Nakupenda Osward!”
“Nakupenda pia!” Walipomaliza kula wakaingia chumbani kulala, ingawa hisia za mapenzi ziliwazidi, lakini Osward aliitia jina la Yesu na kujikuta hisia zote zikipuputika, maneno ya mchungaji yalijirudia akilini mwake. Wakalala wakiwa wamekumbatiana hadi asubuhi, bila kufanya tendo la ndoa. Hata wao wenyewe walistaajabu hali hiyo, waliamini ni nguvu za Mungu ndizo zilizowasaidia.

*********
Mahudhurio ya Jeniffer Kanisani yalikuwa mazuri sana, kitu cha ajabu ni kwamba alikuwa na uwezo wa kushika mafundisho haraka sana. Kwa muda wa miezi mitatu alikuwa akijua vitu vingi sana katika imani ya Kikristo. Alijua kuimba nyimbo mbalimbali, kufungua Biblia na hata kukariri vifungu kadhaa katika Biblia. Osward alifurahi sana.

Baadaye Jeniffer akabatizwa na kuwa Mkristo safi. Mipango ya ndoa ikaendelea kama kawaida. Ndoa yao ikatangazwa Kanisani, huku kamati ikiendelea kushughulikia sherehe ya harusi yao. Watu wote maarufu wa jijini Dar es Salaam walialikwa, wasanii maarufu nao walialikwa kwa ajili ya kutoa burudani kwa waalikwa. Ilitarajiwa kuwa sherehe kubwa ya aina yake. Umaarufu wa Jeniffer na Osward ukaongezeka, ndoa yao ikawa gumzi Dar es Salaam nzima, kila akisema lake.

Ikiwa zimebaki siku kumi kabla ya ndoa yao, Jeniffer alianzisha mjadala wa wapi wataishi baada ya ndoa yao kufungwa, kati ya kwa Jennifer Oysterbay na Mwenge kwa Osward. Ilikuwa ni jioni wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku. Mara nyingi Osward alikuwa akilala kwa Jeniffer, walikuwa kama mtu na mkewe, kitu pekee kilichoondoa maana hiyo ni tendo la ndoa! Walikuwa waangalifu sana na dhambi hiyo.

“Mbona hunijibu!” Jeniffer akamwambia Osward baada ya kumwona ametulia badala ya kumjibu.
“Nikujibu nini Jeniffer?”
“Tutaishi nyumba ipi kati ya hii na ile yako kule Mwenge?”
“Mbona unauliza maswali ambayo tayari yana majibu yake?”
“Yana majibu gani?”

“Mimi ni mwanaume, kwahiyo lazima uje nyumbani kwangu, siwezi kuishi hapa!”
“Kwanini Osward?”
“Kwaababu mimi ni mwanaume, kuishi hapa kwako ni sawa na utakuwa umeioa wewe!”
“Hapana Osward mpenzi wangu, nyumba zote ni zetu, sasa kwanini tusiishi katika nyumba hii ambayo ni nzuri zaidi na ile ya Mwenge tukaipangisha!”

“Tuipangishe siyo?”
“Ndiyo!”
“Kwanini tusipangishe hii, halafu sisi tukaishi Mwenge!”
“Tutaonekana wa ajabu sana kupangisha nyumba nzuri na bora zaidi halafu tukaishi Mwenge, badala ya kuishi pamoja hapa!”
“Hapana, sitaki Jeniffer! Lazima tukaishi nyumbani kwangu!”
“Osward!” Jeniffer aliita.

“Nakusikia!”
“Unanipenda?”
“Ndiyo!”
“Sasa kwani hutaki kuniridhisha mpenzi?”
“Sawa, nimekubaliana na wewe mpenzi wangu! Sipendi kukuudhi, wewe ndiyo mhimili wa maisha yangu!” Baada ya kufikiria sana, Osward aliamua kukubali.

Siku zikazidi kwenda huku pilikapilika za kufunga za harusi zikiendelea kupamba moto, hatimaye siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ikafika! Kanisa lilifurika watu wengi kuliko kawaida, ilikuwa harusi iliyohudhuriwa na watu kuliko harusi yoyote iliyowahi kufanyika kanisani pale.

Kanisa halikutosha, ilibidi maturubali yafungwe nje na kuwekwa viti kwa ajili ya watu kukaa. Baada ya ndoa kufungwa, msafara wa magari ulianza kutokea Kanisani Sinza Mori hadi katika Ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo sherehe ziliendelea hadi usiku wa manane.

Ilipotimu saa tisa za usiku, maharusi wakatoka na kwenda kupumzika Waridi Motel, kila mmoja alikuwa akitamani sana kukutana na mwenzake kimwili. Walipofika chumbani mwao, kitu cha kwanza ilikuwa ni kufanya mapenzi, hawakuchukua muda mrefu kumaliza shughuli hiyo pevu kila mmoja akiwa hajiwezi.

“Osward...” Jeniffer akaita akitweta kwa uchovu.
“Yes darling!”
“Sijawahi kusikia raha kama leo, umenikata kiu yangu ya mapenzi! Wewe ni mwanaume mzuri sana kwangu, sasa nitayafaidi maisha kama msichana mwenye mume kamili!”
“Nashukuru Jeniffer mke wangu, nakupenda sana mpenzi, najivunia kuwa na mwanamke mzuri kama wewe! Wewe ni zawadi yangu kutoka kwa Mungu, nakupenda sana Jeniffer wangu!”

“Hata mimi pia!”
Usiku mzima hawakulala, walikuwa wakifanya mapenzi kama ndio walikuwa wametoka jela, hatimaye alfajiri wakapitiwa na usingizi. Walikuja kushtuka saa tano za asubuhi wakiwa hoi, baada ya kupata kifungua kinywa, kazi ikawa moja mchana kutwa hadi siku mbili baadaye walipopanda ndege na kwenda kupumzika katika Fukwe za Miami nchini Marekani kwa ajili ya fungate lao. Walikaa huko kwa mwezi mzima wakifurahia maisha mapya.
*********
Mwezi mmoja baadaye walirudi Tanzania, ambapo walifikia Oysterbay katika nyumba ya Jeniffer, maisha yakabadilika, wakawa mtu na mkewe. Hakika ilikuwa ndoa yenye furaha sana. Usiku mmoja walikuwa wakipata chakula, Osward alionekana kuwa na mawazo mengi sana, hali iliyomfanya mkewe Jeniffer kuwa na wasiwasi.

“Siyo kawaida yako Osward, lazima kuna tatizo!”
“Hapana mpenzi, ila kuna kitu nataka kukuambia, nasita!”
“Niambie tu mpenzi wangu!”
“Nilikuwa nashauri uache kazi Outreach, tuwe kitu kimoja katika kampuni yangu ili tuweze kusimamia vizuri kampuni!”
“Hujakosea Osward, ni wazo zuri sana, nilikuwa nikifikiria hilo muda mrefu sasa!”
“Ndiyo maana nakupenda!” Osward akamkumbatia Jeniffer na kumtoa kwenye kiti moja kwa moja akampeleka chumbani, yaliyoendelea huko hayaandikiki!

“Osward!” Hatimaye Jeniffer aliita walipomaliza kazi iliyowapeka chumbani.
“Sema malikia wangu!”
“Nina habari nzuri sana kwako!”
“Habari nzuri? Habari gani hizo?”
“Hebu lete mkono wako!” Jeniffer akasema huku akiuchukua mkono wa Osward na kuuweka katika tumbo lake. Osward hakuelewa alikuwa akimaanisha nini.

“Unahisi nini?”
“Mh! Hakuna kitu!”
“Sikiliza Osward, sijaona siku zangu mwezi huu!” Jeniffer alisema akitabasamu.

“Kwahiyo unaaminisha una mimba yangu?”
“Ndiyo...nina mimba yako mpenzi!”
Haikuwa rahisi kwa Osward kuamini, kwanza alibaki ameduwaa kwa nukta kadhaa, kisha baadaye akamkumbatia Jeniffer kwa dakika tano kabla ya kumuachia.

“Nakupenda sana Jeniffer wangu, siamini kama una mtoto wangu tumboni mwako!”
“Amini mpenzi wangu, nakupenda pia Osward, miezi michache baadaye mtoto wetu atakuwa akitusumbuasumbua humu ndani!” Wote wakacheka kwa furaha.

Ilikuwa siku ya furaha sana kwao, ilikuwa zaidi ya siku waliyofunga ndoa. Siku iliyofuata walikwenda kutembelea Mbuga za Wanyama za Mikumi kwa furaha ya Jeniffer kupata ujauzito.

Miezi saba baadaye Jeniffer akajifungua salama mtoto mzuri wa kiume, aliyefanana na Osward kwa kila kitu kasoro macho tu, aliyochukua ya mama yake. Ilikuwa furaha kwa familia nzima. Baadaye mtoto alibatizwa na kupewa jina la Emmanuel yaani Mungu pamoja nasi. Ukurasa mpya ukafunguliwa katika maisha yao, wakaishi maisha yenye furaha yenye kumpendeza Mungu.

MWISHO
N:B Nawashukuru wasomaji wangu kwa kufuatilia hadithi hii kuanzia mwanzo hadi mwisho, naamini kuna jambo mlilojifunza. Hadithi yetu mpya ya The Assassination (Mauaji) itaendelea katika gazeti hili hili siku ya Ijumaa, nimeshindwa kuichapa leo kutokana na ufinyu wa nafasi... MUNGU AWABARIKI SANA!


 (Votes #: 0)
    (17 March 2008)
Soma Zaidi: 612 | Maoni Yako (8)

Udaku Mwingine

hadithi za Shigongo
 
  • MY GHOSTS -36
  • MY GHOSTS (MIZIMU YANGU -25)
  • My Ghosts (Mizimu yangu)(4)
  • My ghosts (Mizimu yangu - 34)
  • My Ghost (Mzimu wangu)(5)
  •    

    #1 Author: Liz Baraka (17 March 2008 09:48)

    Hii ni hadithi nzuri sana, ina mafundisho mazuri kwani watu wengi huangamia kwa kutomkiri Yesu Kristo. Pongezi nyingi.
     
    fast    

    #2 Author: meka (17 March 2008 10:17)

    BIG UP SANA BROTHER,

    HADITHI IMETULIA SANA YAANI NATAMANI ISINGEISHA, LAKINI NI TAMU SANA.

    NATUMAINI NA HII INAYOANZA ITAKUWA BOMBA, MUNGU AKUBARIKI SANA UENDELEE KUTUTUNGIA HADITHI NZURI.

    MAY GOD BLESS U.
     
    fast    

    #3 Author: ashura (17 March 2008 12:45)

    habari yako kaka shigongo nimefurahi sana kumaliza hadithi ambayo tulikuwa tuna wasiwasi juu yetu vp itaendelea, kwa kweli hadithi nzuri na mungu atakuzidishia kipaji ili uzidi kututungia hadithi nyingi na nzuri kuliko izo .god bless u.
     
    fast    

    #4 Author: pendo (17 March 2008 13:12)

    Hongera sana kaka Shigongo kwa hadithi nzuri na ya kuvutia Mungu akubariki zaidi na zaidi ufike mbali zaidi
    Nakutakia kila la kheri katika ujenzi wa taifa letu Tanzania
    Nawaomba watu wote mlio soma hii hadithi kama hujamkiri kama Yesu ni mwana na mwokozi wako anza sasa kwa sababu tumejifunza kwamba Yesu ni jibu ombi bila kukoma utajibiwa maombi Amen.
    Take care
     
    fast    

    #5 Author: Cleophas (17 March 2008 18:13)

    Kaka shigongo mimi nashindwa hata niseme nini,LAKINI UKWELI NI KWAMBA UNATISHA,Kwa utamu wa hadithi hii natamani isingeisha
    Mimi nimejifunza umuhimu wa JINA LA YESU KATIKA HALI ZOTE.NASUBIRIA HADITHI HIYO MPYA KWA HAMU KUBWA.
    MAY GOD BLESS YOU NOW AND THEN!!!!!!!!! love

    Cleophas,
     
    fast    

    #6 Author: bello (27 March 2008 08:19)

    keep up the good work...
    i cant get enough of your stories..
    stay Blessed.
     
    fast    

    #7 Author: msoru (23 June 2008 11:19)

    mimi c msomaji sana wa hadth zako,nasomaga tu kumlizisha rafk yng kwan soma hii soma hii huwa nying.Leo niisoma hii mwanzo had mwisho niona kuna k2 cha kujifunza.Hongera Shigongo pasipo kutarajia waweza fanya m2 akaokoka.
     
    fast    

    #8 Author: hamimu (20 October 2008 15:19)

    Shigongo unatisha mimi ni msomaji mzuri wa hadithi
    zako. Pia ningependa kuona mnatuma vitabu vya hadithi
    hizo mkoani Kigoma kuna watu wengi wanaofuatilia kwa kina hadithi hizo.
    NI HAMIM .J. HAMIM
    WA KIGOMA TZ
     
    fast    

    Add comments

    Name:
    E-mail:

    Code:
    Include security image CAPCHA.
    to renew the code
    Enter Code:

     

    Kura Yako / Poll

    Habari Katika Picha


    Gazeti la Uwazi


    Nani Yupo / Alikuwepo


    Home Page | About Us | Regista | Picha | Bongo Celebrities | Maoni | Contact Us

    hit counter

     

    2008 © globalpublisherstz.com