Hapakuwa na jambo ambalo Gift angeweza kulifanya zaidi ya kukubaliana na matokeo kwamba mama yake alikuwa amekufa na kumfuata pacha wake Grace na kumwacha Gift peke yake duniani! Aliendelea kulia akiwa amekumbatiwa na Sista Adventina, sehemu moja kichwani mwake ilimwambia uamuzi ambao mama yake alikuwa ameuchukua ulikuwa ni wa kichoyo, kwanini alikubali kufa wakati akijua alikuwa akitegemewa? Gift alijiuliza maswali hayo kichwani mwake akiwa amesahau kwamba suala la kifo halikuwa hiari ya mama yake.
“Mama, kwanini umekufa? Kwanini umeniacha?” Aliendelea kulia akiuangalia mwili wa mama yake uliolala kitandani, macho yakiwa yamefumbwa kama vile alikuwa usingizini na muda mfupi tu baadaye angezinduka.
“Gift!” “Bee Sista!” “Umesikia nilivyokuambia lakini?”
“Nimesikia lakini nashindwa kukubali, nampenda sana mama yangu ingawa watu wote walimwona mchawi na malaya na sijui maisha yataendeleaje baada ya hapa, nimebaki peke yangu Sista!” “Hauko peke yako mwanangu Gift unaye Yesu na pia sisi tupo kukusaidia kama tulivyokwishaamua!” Sista Adventina aliendelea kumbembeleza.
Dakika chache baadaye Masista wengi zaidi waliingia chumbani kutoka Makao Makuu yao na kuendelea kumpa pole Gift kwa yote yaliyotokea, miongoni mwao alikuwepo Sista Consolatha, walionekana wazi kuwa katika juhudi za kuyazuia machozi yasiwatoke kwa kuogopa kumuumiza Gift.
Baadaye Gift alishuhudia wauguzi wakimfunga mama yake kwenye mashuka meupe na kumpakia juu ya machela, kisha kuanza kuisukuma kuelekea chumba cha kuhifadhia maiti kilichokuwa umbali wa kama mita mia moja kutoka wodini, Gift alifuata nyuma mpaka kwenye chumba hicho na kushuhudia mama yake akibebwa na kuingizwa kwenye jokofu la kuhifadhia maiti, lilipofungwa ndipo akaanza kuamini kwamba kweli mama yake alikuwa amekufa. Akalia kwa uchungu.
Kutoka hapo alichukuliwa kwenye gari la Sista Adventina na kupelekwa moja kwa moja hadi Makao Makuu ambako shughuli za msiba zilianza, watawa wote waliuchukulia msiba huo kama wa kwao na Kanisa Katoliki kwa sababu Gift hakuwa na ndugu waliotambulika. Mapadri na Masista wengi walikusanyika kumpa pole, ibada ya faraja ikafanyika ndani ya Kanisa Kuu.
Kuwa katikati ya watawa waliomcha Mungu ilimsaidia Gift kupunguza maumivu moyoni mwake, matumaini akawa ameyaweka kwa Mungu na kujikuta akiamini kwamba mama yake alikuwa ametangulia Mbinguni ambako muda si mrefu angeungana naye baada ya kazi yake duniani kukamilika, kazi aliyoamini ni kuwakomboa Watanzania kutoka katika mikono ya viongozi wagandamizaji ambao hawakujali kabisa maslahi ya watu wa chini.
Siku mbili baadaye mazishi yalifanyika kwenye makaburi ya Kanisa, Gift hakuamini mpaka alipoona shimo linafukiwa na baadaye msalaba kuweka juu yake. Alikuwa halii tena, ujasiri ulishamwingia moyoni mwake baada ya kuukubali ukweli. Ibada ilipomalizika, Gift alipiga magoti mbele ya kaburi la mama yake na kuanza kutamka maneno yaliyowafanya hata Masista pamoja na Mapadri wachukue vitambaa vyao na kuanza kujifuta machozi.
“….umekufa mama, Umeniacha peke yangu, Umechagua mwenyewe kumfuata Grace, Moyoni mwangu utabaki, Siku zote za maisha yangu, Nitakumbuka maneno yako,
Hayo yataniongoza daima, Sitafanya mchezo, Kwa bidii nitasoma, Mpaka niitimize ndoto, Uliyoipandikiza moyoni mwangu, Ili nipate kuwaweka huru ndugu zangu,
Wanaoteseka chini ya Mbingu, Nenda mama nenda, Wema mwingi ulitenda, Ingawa binadamu walikutenga,
Kamwe sitakoma kukupenda! Pumzika kwa amani mama!” Aliyasema maneno hayo kama utenzi, watu wote makaburini walianza kulia! Masista wakasogea karibu na kumnyanyua kisha kuondoka naye hadi kwenye jengo lao ambako Gift aliendelea kulia usiku mzima akimkumbuka mama yake.
Masista hawakulala, walilazimika kukesha wakiimba na kusali. Asubuhi ya siku iliyofuata alikuwa na nguvu kidogo lakini hakuruhusiwa kutoka nje na alibaki ndani kwa muda wa wiki mbili, muda wote akiwa na picha ya mama yake mikononi, akiingalia na kukumbuka ambako yeye na mwanamke huyo walitoka. “Zawadi pekee ninayoweza kumpa mama ni kusoma kwa bidii, mpaka nitimize ndoto yangu!”Aliwaza.
Baadaye alirejea katika hali ya kawaida na majibu yalipotoka alikuwa amechaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza katika shule hiyo hiyo ya St. Bernadetha, kazi ikawa imeanza! Gift hakutaka mchezo kwenye somo lake lolote, hakuwa na muda wa kupoteza labda wakati wa Ibada na kuimba. Matokeo ya juhudi hizo yalianza kuonekana kwenye mitihani yake, alikuwa mtu wa kwanza katika kila somo mpaka alipokuwa anamaliza kidato cha nne na kufaulu kwa Dalaja la kwanza yenye pointi saba! Akiwa mwanafunzi aliyefanya vizuri kuliko mwanafunzi yeyote nchini Tanzania.
“Hii ni heshima kwa mama yangu na pacha wangu Grace!” Alisema maneno hayo siku anakabidhiwa zawadi ya kufanya vizuri na Rais wa Jamhuri ya Muungano Ikulu jijini Dar es Salaam.
Watu wote waliomwona kwenye sherehe hiyo walishangazwa na uzuri wake, hakuna binadamu angeweza kumpita Gift bila kusimama na kugeuza shingo yake, ungekutana naye katikati ya usiku akitembea peke yake ungeweza kukimbia ukifikiri labda alikuwa ni jini! Urefu wake, rangi yake ya ngozi, ukubwa wa miguu, wembamba wa kiuno, mipanuko ya nyonga na mengine mengi yalimfanya mtu yeyote asishindwe kusema Gift alipendelewa, alipocheka au kutoa tabasamu ndipo aliwapoozesha kabisa watu, vishimo vidogovidogo kwenye mashavu yake na mwanya katikati ya meno yake, vilikuwa ni kachumbari tosha.
“Wewe mzuri!” Kijana mmoja alimwambia, huyu ndiye aliyefanya vizuri kuliko wavulana wote nchini Tanzania akiwa nyuma ya Gift. “Ahsante, hata mama yangu alikuwa akiniambia hivyo hivyo!” “Hongera sana Gift!” Aliendelea kusema kijana huyo.
“Ahsante, wewe unaitwa nani vile?” “Naitwa Steven, kwetu ni hapa Dar es Salaam, ni mtoto wa mzee Kamuzora!” “Kamuzora tajiri?” “Ndio!” “Nafurahi kukufahamu!” “Mimi pia!”
Gift akaondoka, mbele kidogo aligeuka kuangalia nyuma akimtafuta Sista Adventina ambaye waliongozana naye kutoka Shinyanga, macho yake yakagongana tena na macho ya Steven, wote wawili wakatabasamu! Gift hakuelewa kilichoendelea kwenye moyo wa kijana huyo, wakati wanaondoka kwenda kwenye hoteli waliyofikia bado Steven alikuwa akimwangalia Gift bila kupiga kope, Gift akatabasamu na gari likaondoka.
Baada ya matokeo yake ya kidato cha nne aliamua kubadili mwelekeo, hakutaka tena kuwa mtawa na hilo halikuwa tatizo kwa Masista aliokuwa akiishi nao, walimpa baraka zote. Akajiunga na Shule ya Sekondari ya watoto wenye vipaji maalum ya Kilakala iliyoko Mkoani Morogoro, huo ndio ukawa mwanzo wa Gift kuondoka kwenye Jumba la Masista,
mpaka wakati huo alikuwa hajamjua mwanaume, bikra yake ilikuwa kama alivyokuja nayo duniani! Kitu cha muhimu kwake kilikuwa ni elimu, wanafunzi wa Kilakala walimbandika jina la Msongo, wakimtania alitumwa na kijiji chake.
Hii yote ilikuwa ni kwa sababu ya kusoma sana, hakuwa na muda wa kwenda Mzumbe kucheza disko ingawa wanafunzi wa shule hiyo ya wavulana walipokwenda Kilakala, wengi walikuwa na lengo la kumwona Gift, sifa za uzuri wake zilishasambaa mkoa mzima wa Morogoro, wavulana wengi walimtaka kimapenzi! Hata baadhi ya wafanyabishara wa mji huo hawakusita kupeleka magari yao shuleni hapo siku za kutembelea wanafunzi lakini lengo likiwa ni kumsaka Gift, hakuna aliyefanikiwa mpaka msichana huyo alipomaliza kidato cha sita na kufaulu kisha kujiunga na chuo Kikuu cha Ukonga, jijini Dar es Salaam.
“Haaah! Gift!” “Aaaah! Steven?” “Ndio umenisahau?” “Hapana, ni muda mrefu!”
“Ni kweli, za siku?” “Nzuri!” “Kumbe uko hapa? Nilisikia watu wanajadili mabwenini kwamba kuna msichana mrembo amejiunga, kumbe ni wewe?” “Acha utani Steven, kuna wasichana wangapi wazuri hapa?”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika gazeti hili hili la Championi.
|