Akiongea na Ijumaa, Mpakanjia au maarufu kama ‘Meddy’, amesema kuwa, aliachana na Aisha Bui siku nyingi hata kabla Amina hajafariki dunia tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiria kwamba aliishi naye kwa muda.
Meddy aliyasema hayo alipoulizwa na waandishi wa habari hii kuhusu tuhuma zinazomwandama kwamba, alimuoa Aisha na kumpangia nyumba Mwenge, jijini Dar na baadaye kumtelekeza huku akijua msichana huyo aliaharibu uhusiano wake na baba yake mzazi kwa sababu yake.
Aidha, Meddy aliendelea kuweka wazi kuwa, kikubwa kilichomfanya ampige chini Aisha ni tabia ya ukorofi ambayo yeye alishindwa kuitibu licha ya kumtaka kila wakati abadilike.
“Mimi sijamtelekeza Aisha, ila tabia yake ya ukorofi ndiyo iliyonifanya nitengane naye. Huyo mwanamke ni mkorofi, mkorofi balaa. Si nyinyi wenyewe mliona alivyowatoa baruti na kisu mlipokwenda kumhoji?” Alisema Mpakanjia.
Akionekana hajapendezwa na habari za kudaiwa kumtelekeza Aisha, Mwenge toka kwao Kigamboni, Meddy alisasambua kuwa, kutokana na ukorofi huo, alimtema Aisha hata kabla Amina hajafariki dunia.
Akasema kuwa, aliamua kuchukua hatua hiyo mapema ili kuepusha shari na kwamba, mpaka sasa hana mchumba na ni yeye mwenyewe atakayeamua aishi na yupi lakini siyo Aisha.
Hata hivyo, katika hali ambayo haikutegemewa, Meddy alitoa matamshi yaliyorudisha mambo nyuma pale aliposema kuwa, mpaka anammwaga chini Aisha, hakuwa amefunga naye ndoa kama wengi walivyompakazia. “Mimi sikuwahi kufunga ndoa na Aisha, naapa! Watu walinipakazia tu,” alisema Mpakanjia ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kufungua mambo yaliyofungika kuhusu maisha yake na Amina na Aisha.
Meddy aliongeza kuwa, kuna habari amekuwa akizisikia zikisemwa juu yake, pia amashasikia kwamba, Aisha ana kidume kingine chenye asili ya kiarabu ambacho kinamuua yeye kiaina, lakini yeye hataki kumjibu kitu kwa sababu anajua anataka kusafiria nyota yake au kupata umaarufu kupitia jina lake.
“Nimeshasikia mengi achilia hilo la kumtelekeza, nasikia ana jamaa huyo wa kiarabu na amekuwa akinipaka vibaya mitaani, lakini mimi sijibu kitu, kwani najua anataka kusafiria nyota yangu au kupata umaarufu kupitia jina langu,” alisema Meddy. Aliongeza kuwa, anachokiangalia kwa sasa ni biashara zake tu na si vinginevyo.
Ijumaa lilikwenda nyumbani kwa Aisha, maeneo ya Mwenge baada ya kumkosa kwenye simu, lengo likiwa kutaka kumsikia anasema nini kuhusu madai ya kutoolewa kwa ndoa na Mpakanjia na ukorofi, lakini hakupatikana mara moja. Aidha, Ijumaa lilimtwangia simu dingi wa Aisha, mzee Bui, lakini naye hakuwa tayari kuongelea lolote kuhusu mambo hayo akisisitiza hataki, hataki, hataki kabisa!
|