Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Jumamosi ya wiki iliyopita majira ya saa 3, usiku katika Hosteli ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam iliyopo Mabibo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Uwazi lilipotembelea eneo la tukio liliambiwa kwamba siku hiyo, kulikuwa na Bonanza la michezo lililoandaliwa na SPW (Student Partinership Worldwide) wakishirikiana na serikali ya wanafunzi chuoni hapo (DARUSO) ambalo lilianza saa 9 alasiri na kumalizika saa 3 usiku kwenye viwanja vya mpira vya Mabibo hosteli.
Aidha, taarifa hizo zilieleza kwamba muda mchache baada ya marehemu kutoka mazoezi ya kwaya ya Kanisa la Roman Catholic yaliyokuwa yakifanyika jirani na hosteli hizo, alipita kwenye tamasha hilo ingawa hakukaa kwa muda mrefu kabla ya kwenda kwenye chumba chake namba 250 kilichoko Block C kwa malengo ya kujipumzisha huku akiwaacha wenzake wakiendelea na chereko.
Habari hizo zilieleza kwamba mara marehemu alipofika chumbani alienda kuchukua chakula na maji ya kuoga na aliporejea alifuatwa na mpenzi wake huyo ambaye alimgongea kabla ya kumfungulia ingawa hakumruhusu aingie ndani kwani alisimama ukutani pembeni ya mlango ili kumsikiliza.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinadai kuwa baada ya kuanza mazungumzo nje ya chumba cha marehemu, Mpenzi wake huyo alichomoa kisu mfukoni na kuanza kumchoma nacho na kumfanya aanguke sakafuni na kuvuja damu nyingi.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka kwa mashuhuda, marehemu alichomwa kisu mara tatu kwenye matiti hali iliyomfanya aanguke na kugaragara huku damu zikiwa zimetapakaa sakafuni (kama inavyoonekana pichani ukurasa wa mbele)
Taarifa zaidi zinasema, katika damu hizo zilizokuwa zikitambaa kwenye korido za hosteli hiyo, kulikutwa kisu kilichokuwa kimekatika katika vipande viwili (Kama inavyooneka pichani ukurasa wa mbele) hali iliyoashilia kuwa uchomaji wake ulikumbana na mfupa hivyo kukifanya kishindwe kuhimili hivyo kukatika.
Hata hivyo baada ya tukio hilo ambalo ilikuwa vigumu kushuhudiwa na wanafunzi kwani wengi wao walikuwa kwenye tamasha, muuaji alitoroka eneo la tukio kwa kukimbia hali iliyowashtua baadhi ya wasomi wachache waliokuwa vyumbani hivyo kuanza kumfukuza wakihisia ni mwizi huku wakipiga kelele zilizovuta hisia za watu wengi hivyo kukusanyika.
Katika hali ya kushangaza walimtambua kama mwanafunzi mwenzao ingawa hata hivyo hali aliyokuwa nayo ya hofu na kutweta iliwafanya wamkabe na kumrudisha alikotokea ndipo walipobaini kuwa amefanya mauaji hayo kisha kuanza kumpa kibano kikali ambacho kilimfanya ajeruhiwe na baadaye kutoa taarifa polisi ambao walifika na kumtia hatiani mtuhumiwa.
Aidha, taarifa Uwazi ilizozipata zinasema kwamba mahusiano kati ya wawili hao yalikuwa yamegubikwa na mgogoro mzito uliotokana na marehemu kusitisha uhusiano naye kiasi kwamba Masamba (mtuhumiwa wa mauaji) alikuwa haruhusiwi kuingia chumbani kwa marehemu kama ilivyokuwa zamani kabla ya kuhitilafiana.
Taarifa zilizidi kusema kwamba, wiki moja kabla ya tukio mtuhumiwa baada ya kuona marehemu haoneshi dalili za kurejesha uhusiano wa awali, alikusanya vitu vyake na kuviweka kwenye begi kabla kutaka kujirusha ghorofa ya tatu kwa lengo la kujiua ambapo aliwahiwa na mashuhuda na kuokolewa.
Baada ya tukio hilo la maujai kutokea hofu kubwa ilitanda maeneo ya hosteli huku baadhi ya wanafunzi wakienda kulala kwa ndugu zao walio karibu kwa kuhofia usalama wao.
Naye Kasonzo Sebastian, Katibu wa Kwaya ya Mtakatifu Filomena ya Mabibo Hostel ambaye alikuwa akiimba pamoja na marehemu alisema kwamba, wameshtushwa na kifo hicho na ni pigo kubwa kwa wanakwaya, waumini wa Kanisa la Roman Catholic, wanafunzi wenzake na watu wote kwa ujumla.
Sebastian alisema kwamba, marehemu alikuwa mshirika mzuri katika kwaya na isitoshe Jumapili ya Juni 31, mwaka huu, alienda kufanya kazi ya kuuza Kanda ya albamu yao ya kwanza iitwayo ‘Mbawa za Asubuhi’ shughuli aliyoifanya kwa uaminifu.
Katibu huyo aliendelea kusema kwamba, siku hiyo ya tukio marehemu alifika mapema saa 1:30 usiku katika mazoezi ya kwaya na ilipokaribia saa 3 za usiku wanakwaya waliagana na kila mmoja kuendelea na ratiba yake wakiwa na imani kwamba kesho yake Jumapili (Juzi) wangekuwa naye kuongoza ibada katika Kigango cha Boko, zoezi lililofanyika bila yeye kuwepo.
“Kwa kweli tulipopata taarifa juu ya tukio hilo hatukuamini hadi pale tulipofika katika chumba chake na kumuona akilia kwa maumivu makali ya majeraha yaliyotokana na kisu, Mungu ailaze roho ya marehemu Bertha mahali pema peponi, Amin,” alisema Sebastian kwa uchungu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Mark Kalunguyeye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la Polisi na jana (Jumatatu) alisomewa mashtaka katika mahakama ya wilaya ya Kinondoni huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alikaririwa akisema kuwa tukio kama hili halijawahi kutokea katika historia ya chuo hicho tangu kianzishwe na kuelezea masikitiko yake kwa familia ya wafiwa.


